17/08/2026
Mtoto anayekadiriwa kuwa na miezi minne ametelekezwa katika kituo kidogo cha magari ya abiria yanayosafiri kutoka Babati kuelekea Wilaya ya Hanang' mkoa wa Manyara.
"Ninafanya kazi ya Machinga ya kuuza maji na soda. Jana majira ya saa 10 kuna mama alikuwa amekaa kwenye benchi alikuwa na mtoto mdogo akaniambia ninaomba uniuzie maji nikampa.
-
Akaniambia mtoto wangu analia nataka nimmwagilie maji atakuwa na joto, twende unisaidie kummwagilia. Nikaenda nikamsaidia kule nyuma. Nikamwambia mbona mtoto amepauka leta mafuta tumpake akarudi kuleta mafuta akanipa, nikaona na mimi ni mama ngoja nimpake.
-
Nikampaka mtoto, nikamwambia ni baridi leta nguo tumvalishe. Akanirushia suruali na sweta nikamvalisha nikampelekea nikamwambia gari limekuja chukua mtoto nikauze maji, akamchukua akambeba mgongoni. Baada ya kuuza maji niliporudi akaniambia naomba unishikie mtoto niende msalani nakuja sasa hivi, mtoto alikuwa amelala, nikamshika mama akaenda msalani hakurudi. Kumwangalia simuoni basi ikafika saa 12 nikaenda kuripoti kituoni, nimeenda Ustawi wa Jamii wamenikabidhi mtoto.
-
Ana miezi 4 na ni wa kiume na mimi nina watoto watano. Nilijisikia vibaya hata usiku sikulala, nampa maziwa ya kununua" Amesema Glory Lazaro aliyetelekezewa mtoto.